Katika miongo ya hivi karibuni, dunia imeshuhudia kuongezeka kwa changamoto ya misimamo mikali inayochochea vurugu na ugaidi. Bara la Afrika, sawa na maeneo mengine ya dunia, limeathirika kwa kiasi kikubwa na makundi yenye fikra kali yanayotumia dini, siasa au utambulisho wa kikabila kama kisingizio cha kuhalalisha vitendo vya kikatili. Hali hii imeleta madhara makubwa kwa jamii, uchumi na utulivu wa mataifa.
Ni muhimu kutambua kuwa ugaidi hauanzi kwa silaha, bali huanza kwa fikra. Fikra potofu zinapopandikizwa katika akili za watu -hasa vijana- huweza kubadilika na kuwa fikra kali inayozalisha chuki, migawanyiko ya kijamii, na hatimaye kusababisha vurugu. Kwa hiyo, mapambano dhidi ya ugaidi ni lazima yaanze kwa kupambana na misingi yake ya kiitikadi na kifalsafa.
Nchini Somalia kwa mfano, kundi la Al-Shabaab limekuwa likitumia tafsiri kali na potofu za dini ili kuhalalisha mashambulizi yake dhidi ya watu wasio na hatia, viongozi wa serikali na hata Waislamu wenzao. Kundi hilo hutumia dini kama chombo cha kuwavutia vijana, likiahidi heshima, kipato na malipo ya kiroho. Hali hii inaonyesha wazi kuwa mapambano dhidi ya ugaidi nchini humo hayawezi kutegemea nguvu za kijeshi pekee, bali yanahitaji pia mapambano ya kiitikadi na kielimu.
Kwenye eneo la Sahel - ikiwemo Mali, Niger na Burkina Faso - makundi yenye uhusiano na fikra kali yameendelea kuimarika kwa kutumia migogoro ya kikabila, udhaifu wa serikali na hali ngumu ya kiuchumi. Vijana wengi wasiokuwa na ajira au waliokosa fursa za elimu wamejikuta wakivutwa na propaganda za makundi hayo.
Nchini kama - Nigeria, Chad, na Kamerun- kundi la Boko Haram limeleta maafa makubwa katika nchi hizo. Likiwa limejengwa juu ya tafsiri kali za kidini na upotoshaji wa mafundisho ya Kiislamu, kundi hili limefanya mashambulizi dhidi ya shule, masoko na hata misikiti na makanisa. Jina lake lenyewe lililotafsiriwa kama kupinga elimu ya Magharibi linaonyesha jinsi itikadi potofu zinavyoweza kugeuzwa kuwa chombo cha kuhalalisha vurugu.
Kutokana na mifano hii, ni wazi kuwa mizizi ya msimamo mkali barani Afrika ni mchanganyiko wa sababu za kiitikadi, kijamii na kiuchumi. Hali ya umaskini, ukosefu wa ajira na kutengwa kijamii huchangia kuifanya jamii iwe rahisi kushawishika. Makundi yenye fikra kali mara nyingi hutumia udhaifu huu kuwavutia vijana kwa ahadi za uongo. Kwa hivyo, mikakati ya kupambana na misimamo hiyo lazima ihusishe pia na maendeleo ya kiuchumi, fursa za ajira, na ushirikishwaji wa vijana katika ujenzi wa jamii zao.
Moja ya sababu zinazopelekea kuenea kwa fikra kali ni ukosefu wa elimu sahihi na uelewa mpana wa masuala ya dini na jamii. Wakati vijana wanapokosa mwongozo wa kielimu na kiadili, huwa rahisi kushawishiwa na propaganda zinazoeneza tafsiri potofu za maandiko ya dini au hoja za kisiasa zenye misingi ya chuki. Elimu bora inayojenga fikra huru, uchambuzi makini na maadili ya kuheshimu wengine ni kinga muhimu dhidi ya itikadi kali.
Ni lazima pia kusisitiza jukumu la wanachuoni wa dini na jamii katika kupambana na tafsiri potofu zinazotumiwa kuhalalisha ugaidi. Dini ya Kiislamu inahimiza amani, huruma na kulinda maisha ya binadamu. Basi hakuna mafundisho ya kweli ya kidini yanayoruhusu mauaji ya wasio na hatia au uharibifu wa mali za umma. Kwa hiyo, kuimarisha sauti za wastani na kueneza mafundisho sahihi ni hatua muhimu katika kuzuia fikra kali.
Serikali nazo zina wajibu wa kuunda sera jumuishi zinazolenga kuimarisha haki, usawa na utawala bora. Pale wananchi wanapohisi kunyimwa haki au kutengwa, huzuka mazingira ya chuki na hasira ambayo yanaweza kutumiwa na makundi yenye ajenda za vurugu. Kwa hiyo, haki na usawa ni nguzo muhimu katika kujenga jamii zenye kinga dhidi ya fikra kali.
Vilevile, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina nafasi kubwa katika mchakato huu. Ingawa vinaweza kutumika kusambaza propaganda za chuki na upotoshaji, vinaweza pia kuwa chombo cha kueneza ujumbe wa amani, mshikamano na mazungumzo ya kijamii. Kwa hiyo, ni muhimu kuhakikisha uchapishaji na usambazaji wa habari na taarifa sahihi, kwa uwazi na uwajibikaji, ili kuzuia uvumi na taarifa za kupotosha zinazoweza kuchochea fikra kali.
Kupambana na fikra kali si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii. Familia, shule, taasisi za dini na mashirika ya kiraia zinapaswa kushirikiana katika kujenga kizazi kinachothamini utu wa binadamu, kinachoheshimu na kukubali tofauti za wengine, na kinachotatua migogoro kupitia mazungumzo na njia za amani badala ya vurugu.
Mwishoni, Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Fikra Kali kinaona kwamba kuzuia ugaidi kunahitaji mkakati wa kina unaoshughulikia mizizi yake ya kiitikadi, kijamii na kiuchumi. Kupanda na kuimarisha mbegu za amani, elimu bora na haki ya kijamii ni njia bora ya kuondoa mazingira yanayoruhusu fikra kali kustawi. Jamii inayojengwa juu ya maadili ya huruma, usawa na mshikamano ndiyo ngome imara dhidi ya vurugu na ugaidi. Hivyo basi, ni wajibu wetu sote kushirikiana katika kulinda mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya athari za chuki na misimamo mikali