Siku ya Iddi katika Afrika Mashariki kati ya Mila na Desturi

Imeandaliwa na: Bw. Islam Rajab

  • | Sunday, 22 March, 2026
Siku ya Iddi katika Afrika Mashariki kati ya Mila na Desturi

Siku ya Iddii al-Fitr ni miongoni mwa sikukuu muhimu sana katika Uislamu, inayokuja baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika nchi za Afrika ya Mashariki kama Tanzania, Kenya na Uganda, sikukuu hii inaadhimishwa kwa shangwe kubwa na inaambatana na mila na desturi mbalimbali ambazo zimeathiriwa na utamaduni wa Kiswahili, historia ya Kiislamu pamoja na mazingira ya kijamii ya eneo hilo. Makala hii inalenga kuangazia namna sikukuu ya Iddi inavyoadhimishwa katika nchi hizi pamoja na baadhi ya mila maarufu zinazohusiana nayo.

Kwa Jamii na Waislamu wa Afrika ya Mashariki, Iddi al-Fitr ni siku ya furaha, shukrani na mshikamano wa kijamii. Baada ya mwezi mzima wa Ramadhani, kuswali na kufanya ibada mbalimbali, siku ya Iddi huwa ni wakati wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuwapa uwezo wa kutimiza ibada ya saumu.

Siku hii huanza kwa kuswali Swala ya Iddi, ambayo hufanyika kwa pamoja katika misikiti au katika viwanja vikubwa vya wazi. Baada ya swala, Waislamu husalimiana kwa maneno ya pongezi kama “Eid Mubarak” au kwa Kiswahili “Heri ya Iddi”. Salamu hizi zinaashiria upendo, msamaha na udugu kati ya wanajamii.

Nchini Tanzania, hasa katika maeneo ya pwani kama Zanzibar, Tanga na Dar Es salaam, sikukuu ya Iddi huadhimishwa kwa maandalizi makubwa. Watu huvaa mavazi mapya au mazuri ya kitamaduni kama vile kanzu, kofia na hijabu.

Miongoni mwa vyakula maarufu vinavyoandaliwa siku ya Iddi ni Biryani, Wali wa nazi na mandazi. Familia hukusanyika pamoja ili kula chakula na kuimarisha uhusiano wa kifamilia. Pia watoto hupata zawadi au fedha ndogo ndogo kama ishara ya furaha ya sikukuu.

Katika Kenya, hasa katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu kama Mombasa, na Lamu, Iddi huadhimishwa kwa sherehe kubwa. Baada ya swala ya Iddi, watu hutembeleana majumbani, wakibadilishana chakula na pongezi.

Utamaduni wa Waswahili katika pwani ya Kenya una mchango mkubwa katika maadhimisho haya. Nyumba hupambwa na mara nyingi familia huandaa vyakula vya kitamaduni kama pilau, Samaki na vyakula vya baharini.

Aidha, katika baadhi ya maeneo vijana huandaa mikusanyiko ya kijamii na michezo ya kitamaduni kama sehemu ya kusherehekea sikukuu.

Ama kuhusu nchini Uganda, Waislamu ambao ni sehemu muhimu ya jamii ya taifa hilo pia huadhimisha Iddi kwa shangwe. Miji kama Kampala huwa na mikusanyiko mikubwa ya swala ya Iddi katika misikiti mikubwa au viwanja vya wazi.

Baada ya swala, watu hutembelea ndugu, marafiki na majirani. Mila ya kugawana chakula ni sehemu muhimu ya maadhimisho hayo. Pia, misaada hutolewa kwa maskini ili kuhakikisha kuwa kila mtu anashiriki katika furaha ya sikukuu.

Kwa Waislamu wengi wa Uganda, siku ya Iddi pia ni wakati wa kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza maadili ya Kiislamu kama ukarimu na kusaidiana.

Kwa ujumla, siku ya Iddi katika Afrika ya Mashariki ni tukio muhimu la kidini na kijamii. Ingawa Tanzania, Kenya na Uganda zina tofauti za kitamaduni na kijamii, maadhimisho ya Iddi katika nchi hizi yanafanana katika misingi yake: swala ya pamoja, kushukuru kwa neema ya Ramadhani, kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kusaidiana katika jamii.

Hivyo basi, sikukuu ya Iddi si tu sherehe ya kidini bali pia ni chombo muhimu cha kuimarisha mshikamano, utamaduni na utambulisho wa jamii za Kiislamu katika Afrika ya Mashariki.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.