Uislamu ni dini inayolinda na kuthamini uhai wa binadamu. Miongoni mwa malengo makuu ya Sharia (Maqasid Al-Sharia) ni kulinda nafsi, Kwa sababu hiyo, Uislamu umekataza vikali kuua nafsi bila haki, iwe ni kuua wengine au kujiua mwenyewe. Katika zama za sasa, kuna ongezeko la matukio ya kujiua katika jamii mbalimbali, jambo linalohitaji ufahamu sahihi wa mafundisho ya Kiislamu pamoja na suluhisho madhubuti.
Qur’ani Tukufu inasisitiza heshima ya uhai wa mwanadamu, pale Mwenyezi Mungu S.W Anaposema:" Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni" [Al-Nisaa: 29]. Pia Amesema S.W: “ Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki” [Al-Israa: 33].
Aya hizi zinaonyesha wazi kuwa kuua nafsi ni kosa kubwa isipokuwa katika hali maalum zilizowekwa na sheria, Pia Uislamu unachukulia kuua mtu mmoja kuwa ni sawa na kuua watu wote, Mwenyezi Mungu S.W Amesema: " Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote" [Al-Maidah: 32], Mtume Muhammad S.A.W amesema: “Mwenye kujiua kwa kitu fulani, ataadhibiwa nacho Siku ya Kiyama” (Hadithi sahihi)
Dalili hizi zote zinaonyesha kwamba: Kujiua ni miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu na haramu kabisa anayelifanya tendo hilo ataadhibiwa adahbu kali mwishoni.
Miongoni mwa sababu zinazopelekea watu kujiua ni msongo wa mawazo kwa sababu ya matatizo ya kisaikoloji, kukata tamaa na kupoteza matumain, kuwepo matatizo ya kiuchumi na kijam, upweke na kukosa msaada wa kijamii, na udhaifu wa imani na kukosa mwelekeo wa kiroho. Ingawa hayo, mamabo hayo yote niliyolitaja si hoja ya kujiua nafsi, lakini mtu lazima awe na subira na ridha.
Bila shaka kujiua husababisha madhara makubwa, kama kupoteza maisha ambayo ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu S.W, maumivu kwa familia na jamii, kuvuruga utulivu wa kijamii, na kupunguza thamani ya uhai katika jamii
Njia za Kupambana na tatizo la kujiu
- Kuimarisha Imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu S.W (Tawakkul). Kupitia kumkaribia Mwenyezi Mungu S.W, kusali na kuomba dua, kuamini kuwa matatizo yana suluhisho.
- Kutoa Msaada wa Kisaikolojia, kwa mfano kushauriana na wataalamu wa afya ya akili na kuweka mazingira ya kuzungumza wazi kuhusu matatizo.
- Kuimarisha Mshikamano wa Kijamii, lazima familia na jamii kusaidiana.
- Elimu na Uhamasishaji jambo muhimu sana, kupitia kuelimisha jamii kuhusu hatari ya kujiua na kueneza mafundisho sahihi ya Dini.
- Kutoa Matumaini, kukumbusha kuwa baada ya shida kuna faraja, na kutoa mifano ya watu waliovuka changamoto.
Mwishoni, Uislamu unakataza vikali kuua nafsi na kujiua, kwa sababu uhai ni neema na amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu S.W. Kupambana na tatizo la kujiua kunahitaji juhudi za pamoja za kidini, kijamii na kisaikolojia. Kwa kuimarisha imani, elimu na mshikamano wa jamii, tunaweza kupunguza na hatimaye kutokomeza tatizo hili.