Hija si ibada tu au matendo ya ibada pekee anayoyatekeleza mwenye kuhiji, bali ni ujumbe wa kina unaolenga kumrekebisha mwanadamu na kuhuisha upya uhusiano wake na Mwenyezi Mungu Mtukufu, nafsi yake, na wengineo. Hija ndiyo ibada pekee miongoni mwa nguzo za Uislamu ambayo imepewa jina la sura kamili ndani ya Qur’ani Tukufu, nayo ni "Surat Al-Hajj", ilhali hatuoni sura yenye jina la Swala, Saumu au Zaka.
Je, hija ni safari ya kiroho na ya moyo ambayo mtu huifanya kisha akarudi kama alivyokuwa?
Au ni safari ya kiroho iliyo ya kina zaidi inayomjenga upya mwanadamu kutoka ndani kabisa?
Kwa hakika, hija ni msimu mkubwa wa kila mwaka unaojilea Muislamu katika maadili na maana kuu za kiimani, Muislamu akizihisi kwa uaminifu, anaweza kubadilisha maisha yake kabisa. Kupitia hija, Muislamu husahihisha uhusiano wake na Mola wake, hujirekebisha nafsi yake, huboresha mahusiano yake na watu, na hata hujifunza namna ya kuishi kwa uwiano na ulimwengu unaomzunguka. Hija si mkusanyiko wa ibada za nje pekee, bali ni shule inayomfundisha Muislamu kuyeyusha tofauti za kibinadamu - iwe ni majina, kazi au hadhi za kijamii.
Katika hija, mwanadamu hujivua taswira za uongo za dunia na huelekea katika taswira ya Akhera.
Hija humvua mwanadamu tofauti zote zinazobainisha nafasi yake duniani, kama vile utajiri na umaskini, kabila, rangi na hadhi ya kijamii. Wote huvaa vazi moja, husimama katika eneo moja, hutamka maneno yale yale na kuelekea kwa Mola mmoja. Hapo mwanadamu huanza kuelewa maana kubwa kwamba thamani halisi ya mwanadamu ipo katika uchamungu wake na kurejea kwake kwa Mwenyezi Mungu S.W.
Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema" :Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari" (Al-Hujurat: 13). Katika hija, aya hii haibaki kuwa maandishi yanayosomwa tu, bali hugeuka kuwa uhalisia unaoonekana kwamba watu wote mbele ya Mwenyezi Mungu S.W ni sawa.
Hija pia ni shule ya maadili kabla ya kuwa harakati kati ya alama za Mwenyezi Mungu na ibada. Mwenyezi Mungu S.W Amesema: "Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili!". (Al-Baqarah: 197).
Kutokana na aya hii tukufu tunafahamu kwamba hija si utekelezaji wa matendo ya nje tu, bali ni mafunzo ya vitendo ya kuisafisha nafsi. Katika hija, Muislamu huboresha tabia yake katika nyanja zote za maisha, asifanye maneno machafu: yaani kujidhibiti nafsi katika matamanio na ulimi, asifanye maasi: yaani kujiepusha na uovu na kuvuka mipaka, na asibishane: yaani kujiepusha na ugomvi, hasira na kupaza sauti.
Kwa hiyo, mwenye kuhiji hatakiwi tu kutekeleza ibada, bali anatakiwa kurejea akiwa na maadili bora zaidi, ulimi safi zaidi na moyo wenye utulivu zaidi. Na katika hija pia hujitokeza maana kubwa ya adabu ya mwenye kuhiji kwa viumbe vyote vinavyomzunguka miongoni mwa viumbe hai na visivyo hai, mazingira na maeneo.
Muislamu huonesha adabu kwa Jiwe Jeusi kwa kulibusu si kwa kuliabudu, bali kwa kulitukuza kama alama miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu S.W. Huonesha adabu kwa mahali kwa kutolidhulumu wala kuliharibu, kama Alivyosema Mwenyezi Mungu S.W: " Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu". Vilevile Muislamu huonesha adabu kwa miti kwa kutoikata, kwa ndege kwa kutowatisha, na kwa wanyama wa porini kwa kutowawinda akiwa katika ihramu.
Na katika talbiya ambayo Muislamu huikariri: "Labbayka Allahumma labbayk, labbayka la sharika laka labbayk, innal-hamda wan-ni‘mata laka wal-mulk, la sharika lak". Muislamu huelewa kuwa ni mwito wa kuisafisha moyo dhidi ya dhana ya kujitawala mwenyewe, kumrudisha mwanadamu katika unyenyekevu na kuridhika, na kupunguza kushikamana kupita kiasi na dunia.
Nimeitika, nimeitika Ewe Mola wa Nyumba Tukufu na Haram.. Ewe Mwingi wa neema kwa waja Wako.
Nimeitika, haya makundi ya viumbe yamesimama.. mbele ya mlango wa fadhila Zako.
Kutoka kila pembe wamekuja wakisukumwa na shauku.. Wamehiji na wamejazwa na mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mola wao.
Wametimiza ibada zao, heri kwa wenye ikhlasi miongoni mwao.. Lengo lao ni Mola wao, na machozi yao yamemiminika kama mvua.
Ewe Mwenye rehema kuliko wenye kurehemu, tusamehe pamoja nao.. Na utuondolee misiba yote, Ewe Muumba wa viumbe.