Hijra ya Mtume Muhammad (S.A.W) kutoka Makka kwenda Madina ni miongoni mwa matukio muhimu zaidi katika historia ya Uislamu. Tukio hilo halikuwa tu safari ya kuhamia mahali pengine, bali lilikuwa hatua ya kimkakati iliyolenga kulinda dini, kuhifadhi maisha ya waislamu na kujenga jamii inayojengwa juu ya misingi ya haki, amani na mshikamano.
Kupitia hijra, Mtume (S.A.W) aliweka mfano wa subira, hekima na utegemezi kwa Mwenyezi Mungu. Basi Mtume (S.A.W) alikabiliana na mateso, dhuluma na vitisho kutoka kwa washirikina wa Makka, lakini hakujibu kwa chuki wala uadui dhidi ya watu wasio na hatia. Badala yake, Aliongoza umma wake kuelekea kujenga jamii mpya iliyozingatia maadili mema, kuheshimiana na kuishi kwa amani.
Hijra ya Mtume (S.A.W) haimaanishi tu kuhama kutoka mahali maalumu kwenda pengine. Maana yake pana zaidi ni kuacha maovu na kuelekea katika utiifu wa Mwenyezi Mungu. Mtume Muhammad (S.A.W.) amesema: "Muislamu ni yule ambaye Waislamu wanasalimika na ulimi wake na mkono wake, na muhajiri ni yule anayoyaacha yale aliyoyakataza Mwenyezi Mungu". {Al-Bukhari}
Kutokana na hayo, hijra ni safari ya mabadiliko ya kimaadili na kiroho kabla ya kuwa mabadiliko ya kijiografia.
Hata hivyo, katika nyakati za sasa baadhi ya makundi yenye misimamo mikali yamejaribu kupotosha maana ya hijra. Makundi hayo hutumia dhana hii kuwashawishi vijana kujiunga na harakati za vurugu na ugaidi, wakidai kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kutekeleza mafundisho ya dini. Tafsiri hii ni potofu na inapingana na malengo halisi ya hijra ya Mtume (S.A.W).
Hijra ya Mtume (S.A.W) haikujengwa juu ya umwagaji damu wala kuwadhuru watu wasio na hatia. Badala yake, ilijengwa juu ya kulinda maisha, kuimarisha usalama wa jamii na kueneza maadili mema. Kwa sababu hiyo, haiwezekani kuhusisha hijra ya Kiislamu na vitendo vya ugaidi vinavyosababisha maafa, migogoro na mateso kwa jamii.
Kwa hivyo, ni wajibu wa taasisi za elimu na viongozi wa dini kueleza maana sahihi ya hijra kwa vijana ili kuwakinga dhidi ya propaganda za wenye misimamo mikali. Elimu sahihi ya dini ni ngao muhimu katika kupambana na upotoshaji wa mafundisho ya Kiislamu na katika kuimarisha utamaduni wa amani na mshikamano.
Tunapoadhimisha kumbukumbu ya hijra ya Mtume (S.A.W), tunapaswa kukumbuka kwamba ujumbe wake mkuu ni kujenga jamii bora na kushikamana na maadili ya haki, huruma na amani. Hiyo ndiyo maana ya kweli ya hijra, na huo ndio ujumbe ambao Waislamu wanapaswa kuuenzi.