Matetemeko ya ardhi ni miongoni mwa matukio ya asili ambayo yameendelea kuathiri jamii mbalimbali duniani, yakisababisha vifo, majeraha, uharibifu wa nyumba na miundombinu, pamoja na kuacha athari kubwa za kijamii na kisaikolojia. Wataalamu wa sayansi ya ardhi wanaeleza kwamba matetemeko haya hutokea kutokana na mabadiliko na msukumo unaotokea ndani ya tabaka za ardhi, hasa kutokana na mwendo wa mabamba ya dunia na kujikusanya kwa nguvu katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, mtazamo wa Kiislamu hauoni mgongano kati ya kueleza jinsi tukio linavyotokea na kuamini kwamba Mwenyezi Mungu S.W ndiye Muumba na Mwenye kuendesha ulimwengu. Muislamu anaamini kwamba sababu za kimaumbile ni sehemu ya mfumo ambao Mwenyezi Mungu S.W ameuweka katika ulimwengu.
Na kusema kwamba tetemeko la ardhi lina sababu za kijiolojia hakumaanishi kulikanusha uwezo na matakwa ya Mwenyezi Mungu S.W. Kwa hivyo, kuamini kwamba tukio limetokea kwa qadari ya Mwenyezi Mungu S.W hakumaanishi kuacha kutafuta sababu zake za kisayansi.
Uislamu unamhimiza mwanadamu kutafakari ulimwengu na kutafuta elimu. Qur'ani inasema: "Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili". (Al-Imran: 190). Aya hii inatukumbusha kwamba ulimwengu una mfumo na sheria ambazo mwanadamu anaweza kuzitafiti na kuzifahamu.
Kwa mtazamo huu, pale wataalamu wanapoeleza kwamba tetemeko limetokana na mwendo wa mabamba ya dunia au mabadiliko yanayotokea ndani ya ardhi, maelezo hayo hayaondoi nafasi ya imani. Badala yake, yanaonyesha namna ambavyo mfumo wa ulimwengu unavyofanya kazi.
Kwa Muislamu, sababu haijitegemei yenyewe; sababu ipo kwa uwezo na idhini ya Mwenyezi Mungu S.W. Lakini hapa kuna swali muhimu sana; Je, kila tetemeko la ardhi ni adhabu kwa sababu ya dhambi? Hili ni jambo linalohitaji tahadhari kubwa.
Ni kweli kwamba Qur'ani na Sunnah zinathibitisha kwamba baadhi ya misiba inaweza kuwa matokeo ya matendo ya wanadamu. Mwenyezi Mungu S.W anasema: "Na misiba inayo kusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi". (Ash-Shura: 30)
Lakini aya hii haimaanishi kwamba tunaweza kusema kwa uhakika kuhusu kila tukio fulani kwamba ni adhabu ya Mwenyezi Mungu S.W kwa watu fulani kwa sababu ya dhambi zao. Kwa sababu misiba inaweza kuwa na maana tofauti; Inaweza kuwa "mtihani", inaweza kuwa "onyo na ukumbusho", inaweza kuwa sababu ya mwanadamu kurejea kwa Mola wake, na katika baadhi ya hali inaweza kuwa "adhabu". Lakini kutambua maana maalumu ya tukio fulani kunahitaji dalili, na si sahihi kutoa hukumu ya moja kwa moja bila ushahidi.
Qur'ani inaeleza wazi kwamba waumini watapata mitihani mbalimbali katika maisha yao. Mwenyezi Mungu S.W anasema: "Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri". (Al-Baqarah: 155(
Aya hii inaonyesha kwamba misiba si lazima iwe ishara ya ghadhabu ya Mungu. Mtu mwema anaweza kuathiriwa na ugonjwa, mafuriko, vita au tetemeko la ardhi. Hilo pekee halithibitishi kwamba mtu huyo ni mwenye dhambi au kwamba Mwenyezi Mungu S.W amemwadhibu.
Kwa upande mwingine, mtu anayepata neema na utajiri si lazima awe kipenzi zaidi cha Mwenyezi Mungu S.W. Kwa hiyo, hali ya mtu duniani haiwezi kutumiwa peke yake kupima nafasi yake mbele ya Mwenyezi Mungu S.W.
Pia kuna maswali mawili muhimu sana, la kwanza ni kwa nini watu wema huathiriwa na majanga? Hili ni swali ambalo hujitokeza mara nyingi wakati wa majanga. La pili ni kama ikiwa tetemeko la ardhi ni adhabu, kwa nini linawapata watoto, wazee na watu wasio na hatia?
Jibu la Kiislamu ni kwamba dunia ni mahali pa mtihani, si mahali pa malipo ya mwisho. Mwenyezi Mungu S.W anasema: "Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi". (Al-Mulk: 2(
Kwa hiyo, tukio moja linaweza kuwa na athari tofauti kwa watu tofauti, kwa mmoja linaweza kuwa mtihani wa subira; kwa mwingine likawa sababu ya kusaidia wahanga; kwa mwingine likawa sababu ya kutafakari na kurejea kwa Mwenyezi Mungu S.W.
Kwa hivyo, mwanadamu hawezi kuamua kwa urahisi maana ya ghaibu ya kila tukio, dhambi zinaweza kuwa sababu ya misiba, lakini si kila msiba ni adhabu.
Mtazamo wa Kiislamu unamtaka mwanadamu ajipime na arejee kwa Mwenyezi Mungu S.W anapokumbwa na shida, Mwenyezi Mungu S.W anasema: "Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu". (Ar-Rum: 41)
Aya hii inatoa fundisho muhimu: mwanadamu anapaswa kujichunguza, kutubu na kurekebisha matendo yake. Lakini kufanya hivyo ni tofauti na kuwahukumu waathirika wa janga na kusema: "Mmeathiriwa kwa sababu ya dhambi zenu", Kauli ya aina hii inaweza kuwa ya kikatili na isiyo na msingi wa kutosha wa kisharia, hasa pale inaposemwa kuhusu watu maalumu bila dalili.
Lazima tuseme hapa kwamba sayansi haipingani na imani, wakati mwingine huibuka dhana kwamba kueleza tetemeko la ardhi kisayansi ni kupingana na imani kwamba Mwenyezi Mungu S.W ndiye aliyelisababisha. Hii si sahihi. Sayansi huchunguza sababu zinazoonekana, wakati imani inahusu pia chanzo cha mwisho cha uwepo na mfumo wa ulimwengu.
Kwa mfano, mwanadamu anapougua, anaweza kusema kwamba ugonjwa umetokana na virusi au bakteria. Hilo halipingani na imani kwamba afya na maisha yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu S.W.
Vivyo hivyo, tunaposema tetemeko limetokea kutokana na mabadiliko ya kijiolojia, hatusemi kwamba limetokea nje ya uwezo wa Mwenyezi Mungu S.W, Qur'ani inasema: "Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu". (Az-Zumar: 62)
Kwa hiyo, kutafuta sababu za kisayansi ni sehemu ya kutumia akili ambayo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu.
Ingawa mwanadamu anapaswa kutafuta sababu za kisayansi za matetemeko ya ardhi, majanga haya pia yanaweza kuwa fursa ya kutafakari kuhusu udhaifu wa mwanadamu na ukubwa wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Tetemeko linaweza kumkumbusha mwanadamu kwamba mali, majengo, nguvu na mamlaka haviwezi kumpa usalama kamili, Qur'ani inasema: "na mwanaadamu ameumbwa dhaifu", (An-Nisa: 28)
Udhaifu huu haupaswi kumfanya mwanadamu akate tamaa, bali umfundishe unyenyekevu, huruma na kumtegemea Mwenyezi Mungu S.W pamoja na kuchukua tahadhari zinazofaa.
Mwishoni; matetemeko ya ardhi yanaweza kuelezwa kisayansi kupitia sababu za kijiolojia na kimaumbile, lakini maelezo hayo hayapingani na imani ya Kiislamu kwamba Mwenyezi Mungu S.W ndiye Muumba wa ulimwengu na kwamba kila kinachotokea hutokea kwa qadari na elimu Yake.
Kwa hiyo, ujumbe wa Uislamu mbele ya majanga si wa kueneza hofu, bali ni kuunganisha imani, elimu, tahadhari, subira na huruma. Tetemeko linaweza kutufundisha kuhusu nguvu ya Mwenyezi Mungu S.W, na udhaifu wa mwanadamu na haja yake ya kumrudia Muumba wake.