Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W ni miongoni mwa matukio muhimu katika historia ya Uislamu. Mtume Muhammad S.A.W alitumwa na Mwenyezi Mungu S.W kuwa rehema kwa walimwengu, akaja kuwaita watu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja, kusimamisha uadilifu, kueneza huruma na kuhimiza maadili mema.
Mwenyezi Mungu Anasema: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote..”
(Al-Anbiyā’: 107)
Kwa hiyo, kumkumbuka Mtume S.A.W hakupaswi kuwa tukio la kihistoria pekee, bali ni fursa ya kutafakari juu ya ujumbe wake na namna ya kuutekeleza katika maisha yetu.
Kuzaliwa kwa Mtume S.A.W na mwanzo wa ujumbe wa rehema; Mtume Muhammad S.A.W alizaliwa Makka katika ukoo wa Banu Hashim, katika kabila la Quraysh. Alilelewa katika mazingira ambayo yalikuwa na changamoto nyingi za kijamii na kimaadili, na baadaye Mwenyezi Mungu S.W Akamchagua kuwa Mtume Wake.
Alipofikisha umri wa miaka arobaini, alianza kupokea wahyi kupitia Malaika Jibril A.S, na hapo ukatimia mwanzo wa ujumbe wa Uislamu uliolenga kuwaongoza watu kutoka katika ujinga na dhuluma kuelekea elimu, uadilifu na kumuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja.
Mtume wa maadili mema; Moja ya sifa kubwa za Mtume Muhammad S.A.W ilikuwa tabia yake njema. Mwenyezi Mungu S.W Anasema: “Na hakika wewe una tabia tukufu.”
(Al-Qalam: 4)
Mtume S.A.W aliwahimiza watu kusema ukweli, kutimiza ahadi, kuwaheshimu wazazi, kuwasaidia wahitaji na kuwatendea watu kwa huruma na haki.
Hivyo, kumfuata Mtume S.A.W hakumaanishi kusoma historia yake pekee, bali pia kuiga tabia zake katika maisha ya kila siku.
Rehema kwa wote; Ujumbe wa Mtume S.A.W haukujengwa juu ya chuki au ubaguzi, alisisitiza heshima ya mwanadamu, uadilifu na huruma.
Alisema S.A.W: “Mwenye kutowahurumia watu, Mwenyezi Mungu hatamhurumia.”
Ujumbe huu una umuhimu mkubwa katika dunia ya leo, ambayo inakabiliwa na migogoro, chuki, ubaguzi, fikra kali na vurugu.
Kwa vijana, maisha ya Mtume S.A.W yanatufundisha kwamba nguvu ya kweli haiko katika kuwadharau wengine, bali katika kujizuia, kusamehe, kusaidia na kusimamia haki.
Mtume S.A.W alikuwa anapinga fikra kali, alionya dhidi ya kuzidisha mipaka katika dini, alisema: “Jiepusheni na kupita kiasi katika dini”.
Uislamu unahimiza uwiano, hekima na huruma. Kwa hiyo, yeyote anayatumia mafundisho ya dini kuhalalisha chuki, mauaji au ukatili anapingana na misingi ya ujumbe wa Mtume S.A.W.
Kumfuata Mtume S.A.W kunapaswa kutupeleka katika huruma, wastani, uadilifu na kuheshimu utu wa mwanadamu, si katika chuki na vurugu.
Tunajifunza nini kutokana na maisha yake?
Kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume S.A.W inaweza kuwa fursa ya kujifunza mambo mengi, miongoni mwao: Ukweli na uaminifu katika maneno na matendo, kuwaheshimu wengine hata tunapotofautiana nao, kusamehe pale tunapoweza kulipiza kisasi, kuwasaidia maskini, yatima na wenye mahitaji, kukataa dhuluma na kusimamia haki, kuepuka chuki, ubaguzi na fikra kali, na kuunganisha elimu na tabia njema.
Ujumbe kwa vijana; Vijana ndio nguvu kubwa ya jamii. Wanapokuwa na elimu, maadili na uelewa sahihi wa dini, wanaweza kuwa msingi wa amani na maendeleo.
Maisha ya Mtume S.A.W yanawafundisha vijana kwamba mafanikio ya kweli hayapimwi kwa mali au nguvu pekee, bali pia kwa tabia, uaminifu, manufaa kwa wengine na uwezo wa kusimamia haki.
Katika zama za mitandao ya kijamii, ambapo taarifa na mawazo huenea kwa kasi, vijana wanapaswa kujifunza kutoka katika mwenendo wa Mtume S.A.W kuwa na hekima katika maneno, kuepuka kueneza chuki na kuhakikisha ukweli wa habari kabla ya kuisambaza.
Mwishoni; Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa kiongozi aliyebeba ujumbe wa tauhidi, rehema, haki na maadili mema kwa wanadamu.
Mwenyezi MunguS.W Anasema: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu”
(Al-Ahzāb: 21)
Kwa hiyo, njia bora ya kumuenzi Mtume S.A.W si kumkumbuka kwa maneno pekee, bali ni kufuata mwenendo wake, kuiga tabia zake, kueneza rehema, kusimamia haki na kukataa chuki na fikra kali.
Mtume Muhammad S.A.W alikuwa rehema kwa walimwengu; na kumfuata kwa kweli ni kuifanya rehema hiyo ionekane katika maneno, matendo na mahusiano yetu na wengine.