Kuwezesha Vijana .. Mojawapo ya Mikakati Muhimu ya Kupambana na Ugaidi

Imeandaliwa na Dkt., Hossam Mostafa

  • | Thursday, 24 April, 2025
Kuwezesha Vijana .. Mojawapo ya Mikakati Muhimu ya Kupambana na Ugaidi

 

Katika mazingira ya changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi nyingi duniani, ugaidi unazingatiwa kuwa ni moja ya hatari kubwa zinazotishia amani na maendeleo. Kwa kuwa vijana wanawakilisha idadi kubwa ya watu katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, serikali na mashirika mbalimbali yametambua umuhimu wa kuwawezesha vijana kama sehemu kuu ya mikakati ya kuzuia Fikra Kali na kupambana na ugaidi.

Uhusiano wa Ugaidi na Vijana

Haiwezekani kutenganisha ugaidi na sababu za kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni zinazowakumba vijana. Umaskini, ukosefu wa ajira, kutengwa kijamii, na ukosefu wa uadilifu ni miongoni mwa sababu kuu zinazowafanya baadhi ya vijana kuwa rahisi kushawishiwa kujiunga na makundi ya kigaidi. Vilevile, kukosekana kwa fursa za kujieleza na kushiriki katika maamuzi ya kisiasa huwafanya wengine kutafuta njia mbadala, ambazo huenda zikawa hatari na zenye fikra kali.

Kuwezesha Vijana Kama Njia ya Kupambana na Ugaidi

Kuwawezesha vijana hakumaanishi tu kuwapatia maarifa na ujuzi, bali pia kuwapa fursa ya kushiriki katika kufanya maamuzi, kuwahamasisha kuvumbua mambo mapya, na kuandaa mazingira yanayowahimiza kuwa wabunifu na kushiriki katika ujenzi wa jamii yao. Uwezeshaji huu unakusanya nyanja mbalimbali: kiuchumi kwa kuwapa nafasi za ajira, kijamii kwa kuwaingiza katika shughuli za maendeleo, na kiutamaduni kwa kukuza utambulisho wao na hisia ya uzalendo.

Vijana wanapopewa fursa za kweli za kujitambua na kushiriki katika maendeleo ya jamii, uwezekano wa kujiunga na makundi yenye fikra kali hupungua. Kijana mwenye kazi, anayeheshimiwa, na anayeshiriki katika maisha ya kijamii atakuwa mlinzi wa amani ya jamii yake, si tishio kwake.

Zaidi ya hayo, vijana waliowezeshwa wanaweza kuwa mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi kupitia kuelimisha wenzao, kushiriki katika kampeni za kuelemisha za kuzuia fikra kali, na kuchangia katika utungaji wa sera za kitaifa. Wao ndio wanaoelewa vyema changamoto za kizazi chao, na wana uwezo mkubwa wa kuwafikia wale walio hatarini kushawishiwa na makundi hatari yenye fikra kali.

Ili kuhakikisha kuwa uwezeshaji wa vijana unakuwa na matokeo chanya, Kituo cha Al-Azhar cha Kupambana na Fikra Kali kinapendekeza yafuatayo:

  • Kuweka sera za kielimu zinazojenga fikra ya kiuhakiki na kuwafundisha vijana uzalendo.
  • Kusaidia vijana katika ujasiriamali na mipango ya ubunifu.
  • Kushirikisha vijana katika kutunga sera za kitaifa, hasa zile zinazohusu maendeleo na usalama.
  • Kuimarisha nafasi ya mashirika ya kiraia katika kuendeleza uwezo wa vijana.
  • Kuwalinda vijana dhidi ya fikra kali kupitia uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii, kwa kutokomeza umaskini, kutengwa, na kuendeleza malengo ya maendeleo endelevu.

Mwishoni, kuwawezesha vijana si jambo la hiari, bali ni mkakati wa lazima kwa ajili ya mustakabali salama na thabiti. Kwa kadiri tunavyowekeza katika nguvu za vijana, kuwajengea ujuzi wao, na kuwafungulia milango ya matumaini, ndivyo tunavyoimarisha msingi imara wa jamii unaoweza kupambana na ugaidi kwa ujasiri na ustahimilivu.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.