Kwa mujibu wa hikima ya Mwenyezi Mungu Amehusisha nyakati maalum kwa umuhimu na utukufu wa hali ya juu kuliko nyakati nyingine, ambapo mema katika nyakati hizo huwa marudufu kuliko wakati wowote mwingine, kwani nyakati hizo mahususi zinasifika sana kwa utakatifu na ubora zaidi kuliko wakati wowote, hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu (S.W.) Amezitukuza nyakati hizo na kutukuza vitu vitakatifu na ibada zinazofanywa katika kipindi cha nyakati hizo.
Miongoni mwa nyakati hizo takatifu, Miezi Mitukufu ambayo ni: Dhul-Qiadah, Dhul-Hijja, Muharram na Rajabu, ambayo ni miezi mitatu mfululizo na mmoja peke yake. Mwenyezi Mungu Ameharamisha na kukataza vita kipindi cha miezi hiyo na Akashadidisha ubaya na ukatazo wa dhuluma kwa njia yoyote, kwa hiyo Amesema (S.W.): {Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu} [Al-Tawabah: 36].
Waarabu walikuwa wanadai kutukuza miezi mitakatifu hiyo hata kabla ya Uislamu kwa ajili ya kuwafahamishwa watu kuwa wanaheshimu miezi hiyo na adabu zake, lakini wakati huo huo walikuwa wanachezea miezi hiyo ambapo walikuwa wakitaka kuvamia kabila moja wakati wa mmoja wa miezi hiyo walikuwa wanabadilisha mwezi huo mwaka wanapotaka na kurudishia hali yake ya utakatifu mwaka unaofuata, kwa ajili ya kutimiza mikakati yao wakidhani kuwa wanafanya wema ilhali wanafuata shetani aliyewashawishi wakapotea kwa kuhalalisha Aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu na kuharamisha Aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu (S.W.).
Hali hii ina ishara ya kwamba Mwenyezi Mungu Anastahiki kuabudiwa kwa mujibu wa sheria Aliyoipitisha Yeye siyo kutokana na matamanio ya watu na matakwa yao, kwa hiyo mambo yanayohusu ibada yanategemea sana sheria iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake (S.A.W.) ambapo hiki ndicho kipimo cha usahihi wa ibada na vitendo vinavyofanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kipimo hicho ni kuwa ibada au kitendo kinachofanywa kiwe kinambatana na sheria aliyokuja nayo Mtume (S.A.W.) akiwasilisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake wala siyo kama wanavyotaka watu kwa mujibu wa utashi wao au matamanio yao au udanganyifu ambao wanafanyiwa na shetani.
Kwa hakika fadhila za miezi mitakatifu ni nyingi, kati ya fadhila hizo kwamba mema yanalipiwa thwabu kwa marudufu na vile vile maovu, kwa hiyo Imamu Ibnu Kathiir alisema katika tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mumgu: {Basi msidhulumu nafsi zenu humo} [Al-Tawabah: 36], inamaanisha katika miezi hiyo mitakatifu, kwani kufanya uovu katika miezi hiyo ni baya zaidi kuliko miezi mingine kama yalivyokuwa madhambi katika nchi takatifu (Makkah), ambapo madhambi katika miezi mitakatifu au nchi takatifu huwa kubwa kuliko wakati wowote au mahali pengine, kwa hiyo Mwenyezi Mumgu Amesema: {Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu} [Al-Haji: 25].
Hali hiyo hiyo katika miezi mitakatifu, ambapo madhambi yanayofanywa katika miezi hiyo huwa na mabaya na adhabu marudufu kuliko miezi mingine, kwa hiyo fidia ya mauaji kutokana na madhehebu ya Shafiy na wanavyuoni wengine wengi huwa zaidi kuliko wakati wowote, imesimuliwa kutoka kwa Qatadah kuwa alisema: "Hakika dhulma katika kipindi cha miezi mitakatifu ni kubwa zaidi kuliko dhulma inayotukia kipindi cha wakati wowote mwingine, ingawa dhulma wakati wote hutakikani lakini Mwenyezi Mungu Ameitukuza miezi hiyo kama Anavyotukuza Anayoyataka".
Imamu Al-Qurtubiy alisema: "Msidhulumu nafsi zenu humo katika miezi hiyo mitakatifu kwa kufanya madhambi kwani Mwenyezi Mungu (S.W.) Anapotukuza kitu kwa upande mmoja huwa na utukufu wa upande mmoja na Anapokitukuza kwa pande mbili huwa na utukufu wa pande mbili, kwa hiyo maovu na madhambi yanayohusiana na ktu hicho kulichotukuzwa huwajibisha marudufu ya adhabu, na mema yanayofanywa kwa kitu hicho huwa na thawabu kubwa zaidi, kutokana na hayo yeyote anayetii Mwenyezi Mungu na kufanya mema katika mwezi mtakatifu na nchini takatifu hawi sawa sawa na anayefanya mema haya haya wakati wowote mwingine au pahala pengine"
Kwa hiyo, kudhulumu katika miezi hiyo mitakatifu ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa sababu ya utukufu wa miezi hiyo kwa Mwenyezi Mungu, ambapo miezi hii ina ibada mojawapo ibada kubwa sana katika Uislamu ambayo ni faradhi ya Hajj inayojumuisha ibada zote za kimwili, kimoyo, kifedha, kimaneno, kivitendo na kiitikadi. Na kwa kuwa kuhalalisha vita katika miezi hii kunaweza kusababisha maangamizi ya halaika kwa mahujaji na jamaa zao walioko nyumbani pasipo na dhmbi wala hatia au hata kushirik katika vita, kwa sababu ya hayo Mwenyezi Mungu Alitaka kuwapa watu hawa amani na utulivu wakati wa kufanya ibada hiyo adhimu bali ulimwengu mzima uwe na amani na usalama wakati huo.
Kwa kweli, dini yetu ndiyo dini ya amani na usalama, dini inayokataza mapigano katika thuluthi ya mwaka (miezi minne mitakatifu) kwa lengo la kuwapa watu amani na usalama wa maisha yao, mali na heshima zao. Dini hii pia hairuhusu mapigano ila katika hali ya kujitetea na kujibu uadui tu, ama kinyume na hayo waislamu hawaruhusiwi kuanza mapigano hata na maadui, wala kuwavamia wengine kwa kisingizio chochote. Hakika dini hii imetukuza sana damu ikamzingatia anayefanya uhalifu wa mauaji amepatwa na dhambi kubwa zaidi hasa akfanya uhalifu huu katika kipindi cha miezi minne mitakatifu ambapo dhambi huwa kubwa zidi kuliko wakati mwingineo.
Huu ndio ujumbe wa amani, rehma na usalama kwa ulimwengu wote na kwa wanadamu wote, ujumbe unaotokana na dini hii ya amani na usalama, lakini kwa bahati mbaya wachache tu wanaotambua hivyo.