Umuhimu wa Kuzungumza na Kusikia katika Uislamu

Imeandaliwa na Bw., Eslam Ragab Mohammed

  • | Thursday, 15 May, 2025
Umuhimu wa Kuzungumza na Kusikia katika Uislamu

 

 

Katika jamii nyingi, hasa zile zinazoendelea au zenye mchanganyiko wa tamaduni na dini, hujitokeza dhana mbalimbali ambazo si sahihi kwa msingi wa kielimu, kijamii au kidini. Dhana hizi potofu (au dhana mipaya) mara nyingi huzaliwa kutokana na upungufu wa maarifa, kurithi mitazamo ya kihistoria bila uchambuzi, au kutokana na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na watu wenye maslahi binafsi. Hivyo basi, kuzijadili na kuzikosoa dhana hizi si tu kuwa ni jambo muhimu, bali ni wajibu kwa kila mwislamu.

Uislamu imehimiza juu ya mawasiliano bora, yenye hikma, uadilifu, na lengo la kufikisha ukweli kwa njia inayofaa, ndani ya mawasiliano hayo, kuna vipengele viwili muhimu sana, kuzungumza na kusikia wengine. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mja anapaswa kuwa na hekima na uadilifu katika maneno yake, na pia awe msikivu mzuri wa maneno ya haki, elimu, na mawaidha, vipengele hivi viwili vinaathiri moja kwa moja uhusiano wa mtu na Mwenyezi Mungu, pamoja na uhusiano wake na watu wengine.

Kujadili dhana mipaya kunachochea watu kufikiri kwa kina, kuuliza maswali, na kutafuta majibu ya kina badala ya kuridhika na kile walichokirithi au kusikia. Hii ni njia muhimu ya kukuza fikra huru, ubunifu, na maendeleo ya kielimu katika jamii yoyote, katika makal hii nitabainisha kwa ufupi baadhi ya mambo muhimu kuhusu kuzungumza na kusikia kama vifuatavyo:

Kuzungumza na kusikia huondosha dhana potofu

Dhana potofu huathiri sana uwezo wa mtu au jamii kufanya maamuzi ya busara, pia dhana potofu husababisha upotovu wa itikadi na mwenendo. Kwa mfano, kuelewa potofu kwa aya za Qurani tukufu huweza kuwapelekea baadhi ya watu kuchukua fikra kali, kwa hivyo, ni jukumu la wasomi wa dini na maulama kusahihisha dhana hizo kupitia mafunzo sahihi na mijadala wazi.

Dhana potofu mara nyingi huwa chanzo cha migawanyiko na chuki miongoni mwa wanajamii, dhana zisizo sahihi huweza kuendeleza ubaguzi na kuvunja umoja wa kitaifa, kwa kujadili na kurekebisha dhana hizi, jamii hujifunza kuheshimu tofauti na kushirikiana katika msingi wa ukweli na uadilifu.

Kuzungumza kwa Hekima na Kusikia kwa Makini

Qur’ani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad S.A.W zimeeleza wazi umuhimu wa kutumia ulimi katika njia ya kheri, Mwenyezi Mungu S.W Anasema: "na semeni na watu kwa wema", (Al-Baqarah: 83), pia Anasema: "Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa", (Taha: 44).

Kuzungumza kwa njia ya busara hujenga uhusiano mwema, hufundisha, na hueneza maadili mema, Muislamu anatakiwa ajiepushe na maneno ya matusi au uzushi, kwani ulimi unaweza kuwa chanzo cha dhambi kubwa au malipo makubwa.

Kusikiliza ni sehemu muhimu ya kuelewa na kujifunza, Uislamu umehimiza kusikiliza kwa makini ili mtu aweze kuhukumu kwa haki na kuchukua faida ya maarifa, Mwenyezi Mungu S.W Anasema" :Basi wabashirie waja wangu ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao", (Alzumur: 17-18), pia kusikia kwa makini ni ishara ya unyenyekevu na uadilifu.

Adabu za Kuzungumza na Kusikia

Uislamu umeweka adabu maalum kwa mawasiliano baina ya watu miongoni mwa adabu hizo ni:

Kuzungumza kwa sauti ya wastani na isiyoumiza wengine.

Kutozungumza ovyo bila haja au katika masuala yasiyomhusu mtu.

Kusikiliza wengine bila kuwakatiza au kuwadharau.

Kuepuka kusikiliza maneno ya uongo au chuki.

Mtume S.A.W alisema :"Yeyote anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, basi aseme mema au anyamaze", (Bukhari na Muslim), maneno yana athari kubwa katika kujenga au kubomoa, Uislamu unatufundisha kwamba mtu anaweza kuingia Peponi kwa neno moja jema, au kuingia Motoni kwa neno baya. Vile vile, usikivu mzuri hujenga uelewa, huondoa migogoro, na huongeza mapenzi miongoni mwa Waislamu, kupitia kusikia ndipo mtu huweza kutubu, kujirekebisha, au kufikia hidaya.

Kwa ujumla, kuzungumza na kusahihisha dhana potofu ni kazi ya msingi katika ujenzi wa jamii yenye maarifa, maadili, na mshikamano. Haipaswi kuonekana kama kazi ya kukosoa watu binafsi, bali ni juhudi ya kujenga msingi wa ukweli, hekima, na maendeleo. Viongozi wa dini, wasomi, walimu na wanajamii wote wanapaswa kushirikiana katika kazi hii muhimu ili kuandaa mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwislamu anatakiwa kuwa na tahadhari kubwa katika kutumia ulimi wake na pia awe msikivu wa mambo ya haki na yenye mafundisho. Katika dunia ya leo yenye kelele nyingi na taarifa zisizochujwa, ni wajibu kwa Muislamu kujifunza kusema yaliyo kweli na kusikia yaliyo na maana, kwa lengo la kupata radhi ya Mwenyezi Mungu S.W na kuwafikia watu kwa njia ya hekima.

 

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
5.0

Please login or register to post comments.