Miongoni mwa tabia mbaya zilizoenea katika jamii ya kiislamu hivi karibuni tabia ya ubadhirifu na kutumia pesa kiholela na katika mambo yasiyo na faida kisheria, kwa hiyo maulamaa wa Uislamu wametahadharisha kutoka tabia hii na kubainisha kuwa ni fitina inayoweka jamii hatarini na kusababishia watu matatizo na mateso mengi. Ubadhirifu umekatazwa na Uislamu kwa kuwa tabia hii inasababisha ufisadi kuenea katika jamii, tena ni kuzidisha kiwango cha wastani na inaeleweka kwamba sheria ya kiislamu imekuja na mbinu wa wastani katika mambo yote ya dini na dunia ikikataa kupita kiasi kwa ziada au upungufu.
Kwa hiyo tunaona kwamba sheria ya kiislamu inawahimiza waislamu wawe na mbinu ya wastani katika mambo yao yote ambapo hapo ndipo fadhila hukwapo, kwa mfano ubadhirifu unakataliwa na ubahili pia unakataliwa, lakini mwislamu anatakiwa kuwa na uadilifu na uwastani katika matumizi yake, siyo katika matumizi tu, bali katika mambo yake yote. Mwenyezi Mungu Anawakataza wanadamu wote wasipita kiasi katika chakula kwa kusema: {Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu} [7/31].
Pia, wito wa kuwakataza waislamu wasipita kiasi katika hadithi kadhaa za Mtume (S.A.W.) kama vile kauli yake (S.A.W.): “Enyi Waislamu! Kuleni na kunyweni na vaeni na mtoeni sadaka bila ya kupita kiasi kwa ziada wala kupunguza” kwa hiyo tunaona namna sheria ya kiislamu inavyosisitiza umuhimu wa kufuata mbinu ya kati na kati kwa waisalmu katika mambo yao yote na kutaja haya wazi wazi katika matini za Qurani na Sunna.
Aya na hadithi nyingine za kuwakataza waislamu ubadhirifu ni kama vile kauli yake Mtume (S.A.W.): “Kwa hakika Mola wenu Mlezi Amechukia mambo matatu kutoka kwenu: maneno ya kuwasha fitina baina ya watu, kupoteza mali bure na kuuliza uliza” na pia Mtume ametubainishia kwamba Mwenyezi Mungu (S.W.) Atatuuliza kuhusu mali zetu Siku ya Mwisho kama ilivyokuja katika hadithi iliyosimuliwa na Abdullah bin Masoud kwamba Mtume (S.A.W.) alisema: “Itakapokuwa Siku ya Mwisho, miguu ya mja kabla haijatembea ataulizwa kuhusu mambo matano ambayo amepewa na Mwenyezi Mungu nayo ni: maisha yake ameyatumiaje, ujana wake amefanyaje, mali zake amezichuma kwa namna gani na amezitumia vipi na kuhusu elimu yake amefaidika nayo kwa namna gani?”.
Mbali na maagizo na makatazo yaliyokuja katika sheria ya kiislamu kuhusu ubadhirifu tunaona kuwa elimu ya kisasa imethibitisha usahihi wa mtazamo wa sheria ya kiislamu kuhusu madhara ya ubadhirifu katika chakula, ambapo elimu ya afya ya kisasa imetoa tahadharisho kadhaa kuwakataza wanadamu wasiwe wabadhirifu katika chakula kwa ajili ya kulinda afya yao, kwa hiyo wanavyuoni wanasema kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: {kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu} [7/31] ni jumuisho la matibabu yote. Naye Mtume (S.A.W.) alieleza ukweli huo aliposema: “Kwa kweli mwanadamu hakujaza chombo shari kuliko tumbo lake, afadhali atosheleke kwa vitoweo vya kumsaidia afanya kazi, lakini akiwa hana budi ya kula basi aligawanya nafasi tumboni mwake liwe theluthi kwa chakula, theluthi kwa maji na theluthi kwa kupomoa”.
Kwa hakika ubadhirifu ni tabia mbaya iliyokataliwa na sheria ya kiislamu wala siyo katika chakula na vinywaji tu, bali katika mambo mbalimbali ya maisha hata katika ibada, kwa kuwa dini hiyo ni dini ya ukati na kati inayowahimiza wafuasi wake kutopita kiasi katika jambo lolote mpaka Mtume (S.A.W.) aliwakataza maswhaba zake na waislamu kwa jumla wasipoteza maji ya kutia udhuu ovyo ovyo kwa kusema: “Msifanye israfu katika maji ya kutia udhuu ingawa mkiwa mnatumia maji ya mto yanayotiririka”.
Ama kuhusu ubadhirifu wa mali ambao ni aina mbaya zaidi huwa katika sura mbili: ubadhirifu wa matumizi ya pesa ambao unakataliwa na sheria ya kiislamu hata ikiwa katika sadaka inayosababisha madhara mengine kama ilivyobainishwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo * Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi} [17/26-27]. Pengine aina ya pili ya ubadhirifu ni wa matumizi katika chakula na vinywaji na vitu vingine ambavyo ni kimsingi mahitaji ya maisha lakini kwa kiasi maalumu kwa hiyo kupita kiasi hicho katika matumizi ya mahitaji haya husababisha madhara mengi, kwa hiyo Mwenyezi Mungu (S.W.) Amekataza ubadhirifu wa aina hii pia na kubainisha kwamba wabadhirifu huwa sababu ya kuaangamizwa kwa mataifa na kuporomoka kwa jamii: {Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa} [17/16].