Kwa hakika utukufu wa Uislamu na ustaarabu wake uanajitokeza katika sura na namna mbalimbali za dini hiyo. Na kwa kuangalia Uislamu tunatambua kwamba dini hiyo adhimu imetambulika kwa kusifika kwa sifa maalumu ambazo ni sifa za pekee zinazopambanua dini ya Uislamu kutoka dini nyinginezo.
Na kwa jumla dini ya kiislamu inasifika kwamba ni dini iliyoteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayo vyanzo viwili vikuu; Qurani na Sunna kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu wote kwenye njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema kuisifu dini hiyo kuwa ni dini inayotokana naye Mwenyewe: {Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wakuhisabu} [3/19].
Pia, ni dini ya kijumla maana haikukusudia kundi maalumu la watu au kutoa mafunzo mahususi, bali ni dini ya kujumla inayojumuisha kuwaita viumbe wote wanadamu na majini na kugusia hali zote za maisha duniani na Akhera, hali iliyoelezwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote} [18/49].
Vile vile, dini ya kiislamu ni dini ya kimataifa ambayo ilienea katika sehemu kadha wa kadha ulimwenguni. Ujumbe wa Uislmau hauishii enzi, kizazi wala pahala maaulumu, kwa hiyo Mtume (S.A.W.) amesifika katika Qurani kuwa ni chanzo cha rehma na manai kwa malimwengu wote kama ilivyokuja katika kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote} [25/1].
Ni dini ya kimaumbile inayozingatia maumbile ya mwanadamu na pia ni dini ambayo kila mzaliwa huwa anazaliwa akiwa nayo kisha wazazi wanaweza kumshawishi ajiunge na dini hii au ile, jambo lililoelezwa katika Qurani Takatifu katika kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini -ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui} [30/30].
Pia, ni dini ya uwastani au ukati na kati kwa maana ya kwamba mafunzo na misingi ya dini hiyo yanazingatia uwastani badala ya kufikia mwisho wa jambo kwa upande moja tu, bali huzingatia ukati na kati, wepesi na upole na kukataa upendeleo wowote kwa upande mmoja kuliko mwingine. Maana ya ukati na kati ilisisitizwa katika aya kadhaa na hadithi nyingi za Sunna ya Mtume (S.A.W.), miongoni mwa aya hizo kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu} [2/143].
Uislamu ni dini ya tabia njema na maadili ambapo si jambo la kushangaza kutambua kuwa miongoni mwa misingi ya imani kamili kwa mja ni kuwa na tabia nzuri katika mambo yote na hali zote, kwa kuwa tabia njema ni msingi wa heri za dunia na Akhera, licha ya kuwa ni sababu ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (S.A.W.) ambaye alisifika kwa tabia njema wakati Mwenyezi Mungu Alipotaka kumsifu kwa kusema: {Na hakika wewe una tabia tukufu} [68/4], Mtume aliyefupisha lengo kuu la utume wake katika kulingania tabia njema kwa kusema: “Hakika nimetumwa kwa kukamilisha tabia njema”.
Vile vile, Qurani Takatifu inahimiza sifa na tabia njema na kusimulia visa kadha wa kadha kueleza ubora na utukufu wa tabia hizo, kuhusu ushujaa wa Nabii Mussa (A.S.) na nguvu wake katika haki Mwenyezi Mungu Amesema: {Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana * Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitajiwa kheri utakayo niteremshia * Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka kwenye watu madhaalimu * Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu} [28/23-26].
Kwa kifupi, ustaarabu wa kiislamu katika pande zake zote una sifa maalumu zilizoufanya ustaarabu huo uwe wa aina yake na kudumu kuanzia mwanzo wa dini katika enzi ya Mtume (S.A.W.) mpaka Mwenyezi Mungu Atakaporithi ardhi na yaliyomo juu yake kwa kutegemea misingi imara na mihimili ya dini hiyo ustaarabu huu unaweza kuendelea na kuvuka shida yoyote.