Jamii za leo, chini ya ushawishi wa utandawazi, zinapitia mageuzi makubwa katika elimu, uchumi, teknolojia, tamaduni na maisha ya kijamii. Mageuzi haya yanawagusa vijana moja kwa moja, na kwa bahati mbaya, wengine hujikuta wakiteleza kwenye mitego ya fikra kali.
Athari ya hali hii ni kwamba vijana wanalazimishwa kufuata mtazamo wa kidunia unaopunguza au kuondoa kabisa utambulisho wao wa kidini, na hivyo hubakia Waislamu kwa jina pekee huku vitendo na fikra zao vikiendana na usekula.
Kwa misingi hiyo, ni jukumu lisiloepukika la kidini na kizalendo kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora na kinga dhidi ya makundi yenye fikra kali. Kwa hivyo basi, suala la nafasi ya shule katika kukabiliana na fikra kali linazidi kuwa la dharura
Shule zinapaswa kuwa ngome imara ya malezi bora, zikitoa tahadhari dhidi ya itikadi potofu kupitia mitaala, walimu, mafunzo ya vyombo vya habari na njia mbalimbali za kielimu. Hii itasaidia kulinda usalama wa kifikra wa vijana na kuwakinga dhidi ya ushawishi mbaya.
Wizara ya Elimu inapaswa kuweka msisitizo maalumu kwa shule kuendesha kampeni za uelimishaji na tahadhari dhidi ya makundi ya kigaidi na yenye fikra kali. Juhudi hizi hazipaswi kuachiwa taasisi pekee, bali ni jukumu la pamoja la familia, jamii na taasisi zote za kitaifa kushirikiana katika mradi wa kupambana na chuki na misimamo mikali inayopotosha mafundisho ya Uislamu yenye huruma na msamaha.
Aidha, shule inapaswa kushirikiana kwa karibu na familia ili kutengeneza kizazi kinachoweza kupambana na fikra kali. Kwa kutumia lugha rahisi inayowafikia vijana na kuonyesha hatari ya vurugu na migawanyiko, walimu na viongozi wa shule wanahimizwa kutangaza mazungumzo ya wastani yatakayojenga uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Lengo kuu la juhudi hizi ni kuwalinda vijana dhidi ya kujiunga na makundi ya kigaidi au kupotoshwa na fikra zao. Ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa wanafunzi wa shule na vyuo vikuu ndio walengwa wakuu wa makundi ya kigaidi, hasa barani Afrika, ambako wanashawishiwa kushiriki katika mafunzo na mashambulizi ya kigaidi.
Kituo cha Al-Azhar cha kupambana na fikra kali kimeonya mara kadhaa kwamba Afrika iko katika hatari kubwa kutokana na harakati za makundi ya kigaidi yanayotumia vijana kama nyenzo ya uharibifu. Hivyo basi, bara hili linahitaji mikakati madhubuti ya pamoja kupambana na ugaidi, sambamba na mipango ya kuwarekebisha na kuwarejesha kwenye jamii wale waliopotezwa na fikra za msimamo mkali.