Tabia Njema .. Dhana, Utendaji na namna ya kuzitumia kupambana na fikra potofu

Imeandaliwa na Dkt., Alaa Salah Abdulwahed

  • | Thursday, 27 November, 2025
Tabia Njema .. Dhana, Utendaji na namna ya kuzitumia kupambana na fikra potofu

 

     Inafahamika kwamba ubora wa maisha ya waislamu unategemea kiwango walicho nacho kutoka tabia njema ambazo zina umuhimu mkubwa mno katika dini hiyo, mpaka Mtume (S.A.W.) alijumlisha malengo ya utume wake katika kauli yake: "Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema". Tabia hizo ni kipimo cha kusanifisha jamii na kufanikiwa kwake, ambapo jamii bora ni ile inayofuata maadili ya kibinadamu na tabia njema baina ya watu wake kwa kusifika kwa sifa nzuri kama vile; ushujaa, ukarimu, ukweli, huruma, rehma, uaminifu, uadilifu n.k.

Qurani Takatifu inahimiza sifa na tabia njema na kusimulia visa kadha wa kadha kueleza ubora na utukufu wa tabia hizo, kuhusu ushujaa wa Nabii Mussa (A.S.) na nguvu wake katika haki Mwenyezi Mungu Amesema: {Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana * Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitajiwa kheri utakayo niteremshia * Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwishaokoka kwenye watu madhaalimu * Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu} [28/23-26].

Pia, tunasoma kisa cha Nabii Yusuf (A.S.) na tabia alizokuwa nazo na namna alivyoweza kujiokoa kutoka mtihani mgumu wa Mke wa Bwana wake aliyetaka kumlaghai lakini kwa kuwa tabia yake na sifa nzuri Mwenyezi Mungu Alimwokoa kama ilivyokuja katika Qurani: {Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi} [12/23] Na kwa sababu ya tabia njema na maadili yake Yusuf alipandishwa cheo akawa msaidizi wa mfalme baada ya kuwa mfungwa: {Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na umeaminika * Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi * Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema * Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na wakawa wachamngu} [12/54-57].

Kwa hivyo, tunatambua vipi dini yetu adhimu inategemea na kuzingatia sana tabia njema na maadili mema, mbali na visa vya Manabii na Mitume, tunaona Qurani Takatifu inatoa wito wa kutakasisha tabia na kuchunga maadili kwani ni sababu ya kutukuka kwa umma wowote. Mwenyezi Mungu Amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu,na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, nauovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka} [16/90]. Na tukifuatilia aya za Qurani Tukufu tutaelewa kuwa tabia njema ndiyo msingi muhimu wa umma wetu huu na hakuna dalili lililo wazi zaidi kuliko kumsifu Mtume kwa: {Na hakika wewe una tabia tukufu} [68/4]. Na kauli yake Mtume alipotaka kubainisha lengo kuu la utume wake: "Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema".

Kwa upande mwingine, Qurani Tukufu ilituhadithia kuhusu hatima ya tabia mbaya na ukosefu wa maadili na sifa nzuri na namna ilivyokuwa hali hii sababu ya kuporomoka na kusambaratika kwa jamii na staaraabu nyingi duniani. Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutendamaovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa} [17/16] na Qurani na Sunna imejaa visa vya umma zilizoangamizwa kwa sababu ya tabia zake mbaya, mifano ni kama vile; kaumu wa Manabii Hudu, Swaleh, Luut, Shuaieb na wengine ambao walichafuka kitabia wakastahiki kuadhibiwa duniani na adhabu ya akhera ni kali zaidi.

Aya nyingi katika Qurani zimesimulia visa vya umma hizo, kuhusu kaumu Aad Mwenyezi Mungu Amesema: {Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki,na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi?Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawawanazikataa Ishara zetu! * Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika sikuza ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katikauhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera inahizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa} [41/15-16]

Na kuhusu kaumu wa Nabii Swaleh Mwenyezi Mungu Amesema: {Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha} [27/48] Ama kaumu Luut Mwenyezi Mungu Amesema: {Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo * Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli * Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa!} [29/28-30]

Hali hiyo hiyo ilikuwa na kaumu wa Nabii Shueib kama ilivyosimuliwa katika Qurani Tukufu: {Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwishakufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini * Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi  Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na kumbukeni mlipokuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi} [7/85-86].

Hivyo ndivyo, mtazamo wa Uislamu kuhusu tabia njema na athari ya kuutekeleza katika hali halisi ya maisha ya walimwengu wote kwa jumla na hasa hasa waislamu na jamii za kiislamu.

Mapendekezo kuhusu namna ya kutumia tabia njema kupambana na hali mbaya za jamii za kisasa na uhalifu mbalimbali:

1. Kuimarisha Malezi ya Maadili katika Familia

Familia ndiyo msingi wa tabia. Malezi yenye kusisitiza heshima, uwajibikaji na uaminifu yanajenga vizazi visivyoshawishika kirahisi na uovu. Wazazi watoe mfano bora kwa vitendo, si kwa maneno tu.

2. Kukuza Utamaduni wa Uwazi na Ukweli

Katika jamii zilizo na taarifa nyingi potofu, kusema ukweli na kuthamini uwazi huzuia mifarakano na uhalifu. Mashirika, taasisi na viongozi wawe mfano wa uwazi ili watu watumie maadili kama kigezo cha maamuzi sahihi.

3. Kuweka Misingi ya Kuheshimiana katika Jamii

Heshima inapunguza msongamano wa migogoro: matusi, kejeli, ubaguzi na dharau ndicho chanzo cha uhalifu wa mitandaoni na wa kimwili. Tabia za kusalimiana, kusikilizana na kujali zinatengeneza mazingira salama na yenye mshikamano.

4. Kukuza Tabia ya Kujitolea na Msaada kwa Wengine

Jamii yenye moyo wa kusaidiana hupunguza shinikizo la kiuchumi linalosukuma watu kwenye uhalifu. Makundi ya vijana yahamasishwe kujitolea kwenye usafi wa mazingira, kutembelea wagonjwa, kusaidia wahitaji na miradi ya kijamii.

5. Kuelimisha Jamii Kuhusu Matumizi Sahihi ya Mitandao ya Kijamii

Uongo, uchochezi na udhalilishwaji mtandaoni hushamiri pale watu wanapokosa misingi ya maadili. Kufundisha tabia ya kuheshimu faragha, kuepuka matusi na kusambaza taarifa sahihi kunazuia uhalifu wa kimtandao.

6. Kuendeleza Utamaduni wa Kufanya Kazi kwa Uadilifu

Uzembe, rushwa na ujanja ujanja katika ajira huchangia uharibifu wa mifumo ya kijamii. Tabia njema za kutumia muda vizuri, kutenda haki na kutochukua visivyo halali huimarisha uchumi na kupunguza uhalifu.

7. Kusimamia Hasira na Kukuza Staha

Idadi kubwa ya makosa ya jinai hutokana na kutokujizuia. Elimu ya afya ya akili, mitazamo chanya na mafunzo ya udhibiti wa hasira ni njia ya kuzuia vita vya familia, majirani na uhalifu wa mitaani.

8. Kujenga Uaminifu Kati ya Jamii na Vyombo vya Usalama

Watu wenye tabia njema na uwajibikaji hushirikiana na taasisi za usalama kutoa taarifa za uhalifu. Mahusiano mazuri yanajenga mazingira ambayo wahalifu hawawezi kujificha kirahisi.

9. Kuimarisha Nidhamu ya Kibinafsi

Nidhamu ya kufuata sheria, kuheshimu muda, kutunza mali za umma na kujiepusha na tamaa kupita kiasi ni msingi wa kupambana na uhalifu. Watu wanaojiendesha kwa nidhamu huwa na ushawishi chanya kwa wengine.

10. Kukuza Mazingira ya Mazungumzo na Suluhu Badala ya Ugomvi

Badala ya kulipiza kisasi, tabia ya kusikiliza, kuomba msamaha na kusamehe hupunguza chuki ambazo mara nyingi huzaa uhalifu.

Print
Categories: Makala
Tags:
Rate this article:
No rating

Please login or register to post comments.