Ukatili dhidi ya wanawake unaendelea kuwa tatizo kubwa linaloathiri jamii nyingi barani Afrika. Licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na mashirika ya kijamii, wanawake wengi bado wanakumbana na dhuluma za kimwili, kijinsia, kiuchumi, na kisaikolojia. Madhara ya ukatili huu hazikomi tu kwenye maumivu ya kibinafsi, bali pia huathiri familia nzima, jamii, na hata usalama wa taifa. Katika baadhi ya maeneo, ukatili huu umekuwa mojawapo ya sababu zinazowasukuma baadhi ya wanawake kujiunga na makundi yenye fikra kali na ya kigaidi, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.
Wanawake wanaopitia ukatili mara nyingi hutengwa na jamii au kushindwa kupata msaada unaohitajika kutoka kwa taasisi za kisheria na kijamii. Pale wanapokosa mahali pa kukimbilia, wanabaki wakiwa na majeraha ya kimwili na ya kisaikolojia ambayo hayajatibiwa.
Makundi yenye misimamo mikali, kama vile al-Shabaab, Boko Haram, na makundi mengine, hutumia hali hii ya udhaifu kama ni fursa ya kuwavuta wahasiriwa hao. Kwa kuwa makundi haya mara nyingi huwaapa ahadi za ulinzi, makazi, au nafasi ya kuanza upya, wanawake waliokata tamaa wanaona haya kama ni njia ya kuokoa maisha yao au kupata heshima walizoikosa.
Zaidi ya madhara ya kimwili, ukatili huathiri vibaya hali ya kisaikolojia na kihisia kwa mwanamke. Waathirika wa dhuluma ya muda mrefu mara nyingi hupoteza imani katika mfumo wa serikali na jamii yao, jambo ambalo huwafanya wawe rahisi kusukumwa na propaganda zinazowahimiza kujiunga makundi yanayopingana na serikali. Hasira, kukata tamaa, na hamu ya kulipiza kisasi zinaweza kuwafanya wanawake kuwa rahisi kutumiwa kama chombo cha kufanikisha malengo ya kigaidi.
Aidha, ukatili dhidi ya wanawake mara nyingi huchangia kueneza umaskini kwa wanawake. Katika jamii nyingi za Kiafrika, ukatili huu huwa unahusiana na kunyimwa haki ya kumiliki mali, kupata elimu, au kufanya kazi.
Mwanamke anayekosa uhuru wa kiuchumi na anayemtegemea mwingine kifedha huwa katika mazingira ya hatari na udhaifu mkubwa, jambo linalomfanya awe rahisi kuvutiwa na makundi yenye misimamo mikali. Kwa kuwapa mahitaji ya msingi kama vile chakula, fedha au ulinzi wa kiuchumi, makundi hayo huwashawishi wanawake wasiokuwa na njia mbadala za kujipatia riziki.
Hali hii ya kudharauliwa na kuteswa kifamilia na kijamii huwasukuma wanawake kutafuta utambulisho mpya, au kujaribu kujitengana na maumivu ya yaliyowapata. Katika mazingira hayo, wanawake wengine hutumiwa kama wafanyakazi wa nyumbani, wabebaji wa silaha, au hata kushirikishwa moja kwa moja katika vitendo vya kigaidi bila uelewa wa kutosha kuhusu hatari kubwa zinazowakabili.
Hivyo basi, ukatili dhidi ya wanawake haukiuki tu haki za binadamu, bali pia unakuwa njia rahisi ambayo makundi ya kigaidi hutumia kuwavutia wanawake ili watekeleze malengo yao mabaya.
Ili kukabiliana na changamoto hii kwa ufanisi, ni muhimu kukabiliana na chanzo chake, ambalo ni ukatili dhidi ya wanawake. Hii inahitaji elimu ya haki za wanawake, kuimarisha sheria zinazolinda wanawake, kutoa huduma za usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, kujenga uchumi jumuishi unaowawezesha wanawake kujitegemea, na kuhakikisha waathiriwa wanapata makazi salama na msaada wa kisheria bila hofu au aibu.
Mwishowe, Kutetea haki, usalama, na ustawi wa mwanamke si tu juhudi za kijinsia, bali ni msingi wa kujenga jamii yenye amani, uthabiti, na maendeleo barani Afrika.